Abasia
Utume wetu Msumbiji | Abasia
Utume wetu Msumbiji
Utume wetu Msumbiji
Abbey / Utume wetu Msumbiji

Miaka zaidi ya mia moja iliyopita wamisionari Wabenediktini walifika mara ya kwanza Tanganyika na kuanza kazi ya kueneza Injili. Hii ilikuwa mwaka 1894 wakati Padre Maurus Hartamann OSB alipoanza kazi yake kusini mwa mto Rufiji. Ni wazi kwamba mwanzo ulikuwa ni mgumu, lakini hatua kwa hatua kazi yao ilizaa matunda. Matokeo yanaonekana kwa sasa ni majimbo ya Mtwara, Lindi, Tunduru-Masasi na Abasia yenyewe ya Ndanda.

Leo hii Ndanda ni zaidi ya misioni. Baada ya majimbo yaliyotajwa hapo juu kuanzishwa, Ndanda imejirudi na kuwa tena monasteri ya Kibenediktini ambayo lengo lake (kimsingi) si kuanzisha na kuendesha maparokia kama ilivyokuwa siku za nyuma. Hata hivyo katika kutambua wito wetu wa kimisionari hivi karibuni tulikata shauri kuanzisha kituo kipya cha kimisionari nje ya Tanzania, yaani Awasse, Msumbiji. Wamisionari wa kwanza walienda kwa mara ya kwanza huko mwaka 2014.

Nyumba hii mpya ya kitawa iliyopo Awasse (Nango) inakusudiwa kuwa kituo muhimu katika shughuli zetu za kimisionari huko Msumbiji. Kwa kuishi kimonaki, tunakusudia kuiishi kivitendo maisha ya kitawa kadiri ya Mt. Benedikto kwa kusali na kufanya kazi pamoja. Kwa kufanya kazi parokiani tunapenda kuitikia wito wetu kama watawa ambao ni wamisionari pia. Mipango iko mbioni pia kujikita katika kutoa huduma nyinginezo za kijamii hasa katika sekta ya afya (hospitali) na pia katika kufundisha vijana (ufundi).
Wakati kazi zote za kuanzia zitafanyika na ndugu kutoka Tanzania, ni dhahiri kwetu kwamba maendeleo ya misioni hii itawategemea sana wananchi wa Msumbiji. Kwa sababu hiyo mipango ipo mbioni kabisa kuanza kuwapokea vijana wanaoonesha moyo wa kujiunga nasi. Mara tu miundo mbinu ya kimalezi itakapokamilika, tunategemea kuanza kuwatayarisha vijana ambao siku za usoni wataweza kushirikiana nasi katika kusukuma mbele gurudumu la misioni hii ya Msumbiji.