TANGU MWANZO Ndanda imekuwa inatoa mchango mkubwa katika kuwaelimisha vijana katika kada mbalimbali. Wajibu huo kwa sasa umeimarishwa na kupanuliwa ili kukidhi mahitaji ya vijana wa wakati wetu. Mfano wake ni:
- Chuo cha Ufundi Ndanda: chuo hiki kina uwezo wa kuchukua vijana wa kike na wa kiume Zaidi ya 150 kwa mwaka. Hawa hujifunza na kufuzu (kadiri ya viwango vya VETA) katika kada hizi: umeme, magari, useremala, ujenzi, ushonaji, ufundi bomba, ufundi chuma, uchapishaji, kompyuta, n.k.
- Chuo cha Uuguzi Ndanda: Chuo hiki kimeunganishwa na Hospitali yetu ya Ndanda. Vijana wanaosoma hapa hufuzu kwa kiwango cha diploma na wanapata nafasi nzuri ya kujfunza kwa vitendo hospitalini. Wamalizapo huweza kupata kazi katika hospitali yetu au katika hospitali nyingine.
- Sekondari ya Wavulana ya Abbey: Ni vigumu kwa jamii yoyote kufanya maendeleo ya maana bila kuwekeza katika elimu. Kwa kutambua hilo, jumuiya yetu inaendesha shule hii ambayo vijana wanaweza kusoma kuanzia kidato cha kwanza hadi cha sita. Shule ina uwezo wa kuchukua vijana kama 600 hivi. Tunaona fahari kwamba shule hii ipo kati ya zile zinazofanya vizuri zaidi kitaifa.
- Shule ya Msingi ya Abbey: Tunaamini kuwa mtoto lazima apate elimu nzuri mapema iwezekanavyo. Kwa kuanzisha shule hii, lengo letu ni kumwezesha mtoto tangu akiwa na miaka mitano hivi (awali) aweze kupata msingi bora wa elimu. Shule hii inatoa elimu ya awali na ya msingi kwa lugha ya Kiingereza. Vyuo na shule zetu hizi husajili na kupokea vijana kila mwaka.