MALAIKA WALIPOWATOKEA Wachungaji wa Bethlehemu siku ya kuzwaliwa Bwana waliwaambia: “Nawaletea habari njema ya furaha kuu… Kwa ajili yenu mtoto amezaliwa…” Kupata mtoto, katika utamaduni wowote ni sababu ya furaha na mara nyingine shangwe kubwa kabisa. Ni ishara ya baraka,  ni alama ya mafanikio. Abasia ya Ndanda imekuwepo zaidi ya miaka themanini iliyopita. Shughuli zetu za kimisionari hadi hivi karibuni zilijikita zaidi hapa hapa nchini. Mtazamao huo umebadilika hivi majuzi baada ya kuamua kuvuka mpaka na kufungua misioni mpya nchini Msumbiji.

Hakika tarehe sita Oktoba ya mwaba 2019 itakumbukwa daima katika historia yetu, historia ya shirika na katika historia ya Kanisa la Msumbiji kwa ujumla. Kwa mara ya kwanza wanmisionari wa shirika letu wanakanyaga ardhi ya Msumbiji kwa lengo la kushirikiana na Wanakanisa wa kule pamoja na jamii nzima katika kukuza, kuendeleza na kusukuma mbele maisha tenganifu ya watu. Ni baraka kwetu na tunamshukuru Mungu kwa hii.

Kama matayarisho ya uptime huu, ndugu wanne waliteuliwa na kutumwa kuanzisha kazi hii muhimu. Hawa walivuka mpaka na kuingia Msumbiji mwaka 2014.  Kundi hili  la kwanza lilikuwa na ndugu wafuatao:  Pd. Valentino Kaniki, Pd. Jorge Bianco, Bro. Theobald Bayyo na Bro. Bosco Bainit. Kufika tu, iliwapasa kujifunza kwanza Kireno na baadaye kuanza maisha ya jumuiya na ya uchungaji katika parokia ya Mocimboa. Wakiwa pale matayarisho ya kupata eneo kwa ajili ya kujenga monasteri yalianza.  Kwa bahati nzuri eneo lilipatikana katika kijiji cha N’nango. Ujenzi wa monasteri ulianza. Mnamoo Oktoba, (mwezi wa misioni) 2019 siku ya tarehe sita – misioni hiyo ilizinduliwa rasmi.

Tukio hilo lilishuhudiwa na maaskofu wawili na pia maabate wawili. Watawa wa mashirika mbalimbali ya kiume na kike yaliwakilishwa pia katika tukio hilo la kihistoria. Kilichofurahisha zaidi ni ushiriki wa mamia na mamia ya Wakristu na Wanakijiji wa ujirani. Ushiriki wao unatukumbusha ukweli huu: tumekwenda Msumbiji kwa ajili ya watu. Imekuwa dhahiri kwetu kwamba watu wamethamini ujio wetu na kwamba wanategemea mchango wetu katika uchungaji na katika maisha yao kwa ujumla. Kujitoa kwao katika kufanikisha tukio hilo kumetufundisha kuwa watu hawa wana kiu na wako tayari kushirikiana na Wamisionari wetu.  Kwa upande wetu tunasema kwamba, watu wetu ndio nguvu yetu. Na bila wao, hata kwenda kwetu Msumbiji kusingekuwa na maana. Ni matumaini yetu kuwa ushirkiano wetu na watu wetu utawezesha kazi yetu iweze kuleta matunda yanayotarajiwa.

Ibada na mashangilio yalifungwa mnao saa kumi na moja jioni. Ndani ya muda mfupi wageni wote walikuwa wamerudi makwao na watawa wachache waliokuwepo walijikuta  peke yao. Hili lilinitafakarisha na jambo moja lilikuwa bayana kwangu: SHEREHE ZIMESIHA. KAZI IMEANZA!

Pd. Christian OSB – Ofisi ya Misioni ya Abasia