Kwa masikitiko makubwa, jumuiya ya Abasia Ndanda inatangaza kilo cha Mmisionari  mashuhuri na wa muda mrefu, Fr. Witamr Mezger OSB.

Baba Witmar Metzger OSB  (pichani) alizaliwa tarehe 23 Juni 1930  katika Wilaya ya Main-Tauber, Baden-Würtenburg, Ujerumani. Wazazi wake walikuwa wakulima Bw. Alfons (mkulima) na Bi. Agatha Metzger (alyekuwa mama wa nyumbani). Wazazi hao walijaliwa watoto watatu, wavulana wawili na dada mmoja. Wa kwanza wao ni Albert ambaye aliingia utawani na kupewa jina Witmar.

Kati ya 1937-1941, kijana Albert alipata elimu yake ya msingi huko Gerlachsheim. Hii ilifuatiwa na elimu ya sekondari kati ya 1941 – 1946 huko Tauberbischofsheim. Baada ya shule yake ya sekondari aliingia Seminari ya St. Benedict, Würzburg, kati ya mwaka 1946-1949. Kijana Albert alisoma ama wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia au kabla yake. Familia yake ilikuwa mojawapo ya wahanga wengi wa vita hii ya pili ya dunia. Alikulia katika mazingira magumu ya kujenga upya Ujerumani ambayo ilikuwa imeharibiwa na kubomolewa na mabomu ya Nchi-Shirika zilizopigana na Ujerumani wakati huo. Maisha yalikuwa magumu bila fedha wala chakula cha kutosha. Katika hali hiyo kijana Albert alijifunza na kuelewa maana ya umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii katika maisha. Tabia ya kijana Albert kufanya kazi kwa bidii ilidhihirishwa, sio tu kwa kuwasaidia wazazi wake katika shamba lao dogo, bali katika maisha yake yote kama mwanafunzi mtawa na mmisionari.

Kijana Albert alijisikia wito wa kumtumikia Mungu kama Mtawa, hivyo mwaka 1949 alipiga hodi Abasia ya Münsterschwarzach kwa lengo la kujiunga na utawa. Katika malezi alipewa jina jipya la Witmar.  Kati ya Oktoba 1950  na 1955 Bro. Witmar alisoma Falsafa  na Teolojia huko St Ottilien. Mwaka huo huo, 1955 alipewa daraja la Upadre na Abate Askofu Ebehard Spieß wa Peramiho huko Münsterschwarzach. Baadae alifanya masomo ya Uzamifu katika Teolojia huko Roma hadi 1957

Mwaka 1958 – 1959 alienda chuko kikuu cha London Uingereza na kutunukiwa cheti cha Ualimu. Baada ya hapo, ndipo ile ndoto yake ya kuwa Mtawa mmisionari ilipotimia kwani,  tarehe 13 Septemba 1959 Pd. Witmar alitumwa Ndanda kama mmisionari. Mara baada ya kuwasili Ndanda, alianza moja kwa moja kufundisha Hisabati katika shule ya sekondari ya Ndanda; kazi ambayo aliifanya kwa kipindi cha mwaka mmoja tu.

Kutoka mwaka 1961 – 1968, Pd. Witmar alikuwa prior wa Abasia ya Ndanda. Licha ya kuwa Prior, Baba Witmar alifanya kazi nyingine katika ofisi ya Utawala, na idara ya elimu ya Abasia (Nullius)  ya Ndanda wakati ule.  1968 – 1975, Pd. Witmar alifanya kazi za kichungaji huko Mkowe na Mbekenyera. Kazi ambayo aliifanya kwa weledi na kwa juhudi kubwa kama mchungaji mwema.

Kutoka 1975 hadi 2010, Pd. Witmar alifanya utume katika Jimbo la Mtwara. Alifanya kazi nyingi ambazo itakuwa ngumu kuzikumbuka na kuzitaja zote. Alikuwa mhasibu wa Jimbo, mchora ramani wa majengo, mjenzi na mkarabati wa makanisa na majengo mbalimbali ya jimbo na pia alifanya kazi za kichungaji parokiani. Alilfanya kazi hizi kwa muda wa miaka 35. Baadhi ya makanisa aliyojenga ni pamoja na Shangani West, kanisa la Mt. Joseph Newala, kanisa la Tandahma, Namombwe, Ruangwa, Mbekenyera, Kanisa la Mwena. Amejenga vigango kadhaa, kurabati makanisa na nyumba za parokia, chekechea, n.k. Alikuwa mtu muhimu katika upatikanaji wa shamba la Narunyu ambalo hapo baadaye Novisiati ya Masista wa Ndolo iliejengwa. Ni mchoraji na mjenzi, pia, wa majengo ya sekondari ya Masista na Aquinas,  Mtwara.

Pd. Witmar alikuwa mtu wa vipaji vingi. Ingawa alikuwa na msomi aliyebobea katika  Theolojia, hakujishughulisha na ufundishaji wa somo hilo seminari kuu. Hakuwa tu mwana hisabati, bali msanifu wa kujitegemea na mhandisi wa majengo. Alibuni na kusimamia ujenzi wa miradi yote iliyotajwa hapo juu bila majivuno na bila kudai heshima ya pekee. Hakika baba Witmar alikuwa mtu mnyenyekevu.

Baada ya kazi zake hizo za kutukuka Pd. Witmar alirudi Abasia mwaka 2010. Kwa hakika ingewekuwa muda wake wa kustaafu na kupumzika. Hata hivyo Pd. Witmar hakufanya hivyo. Mwaka 2011 – 2013 alitumwa Sakharani (Jimbo la Tanga) ambako alikarabiti majengo mbalimbali. Pia alijenga  jingo la utawala na pia miundo mbinu ya usambazi maji.

Mwaka 2013 alimaliza kazi yake huko Sakharani na kurudi Ndanda. Hata hivyo roho yake ya umisionari iliendelea kumsukuma kufanya kitu. Kipindi hiki wazo la kufungua misioni huko Msumbiji lilizaliwa. Katika uzee wake wa miaka 80, Pd. Witmar alisema yupo tayari kwenda kwenye misioni mpya. Alikuwa tayari kujifunza Lugha ya Kimakonde na Kireno kwa misioni hii mpya. Alijifunza lugha hizo kwa juhudi hadi kuweza kusali na kuadhimisha misa katika lugha ya Kireno.

Licha ya mafanikio  katika Lugha, Pd. Witmar alijenga Kanisa jipya katika Parokia ya Imbuho huko Msumbiji. Pia alijenga nyumba ya mapadre, shule ya Chekechea na kufanya mpango wa kupata kiwanja kwa masista wa Ndolo kwa lengo la kuanzisha nyumba ya kitawa. Kiwanja alipata lakini hakufaulu ujenzi wa makazi haya  kutokana na changamoto za usalama Msumbiji na pia kutokana na afya yake.

Mnamo Aprili 2020, afya yake ilidhoofu kutokana na uzee na maradhi nyemelezi. Hivyo mwezi April alirudi rasmi hapa Ndanda. Afya yake ilizidi kudhoofu na ndipo Oktoba 2020, alihamishishiwa katika nyumba ya kutunza Wazee ya Masista wa Tutzing. Akiwa pale alitunzwa kwa upendo wa hali ya juu na masista hao. Tar 17 Julai 2021, ilibidi Pd. Witmar apelekwe Hospital kwa uangalizi zaidi na wa karibu wa kitabibu.

Pd. Witmar alikuwa mtu mwenye vipaji vingi.  Alikuwa mtu wa akili nyingi, imani ya kina na mtu wa vitendo. Alikuwa mwalimu, mchungaji, kiongozi, msanifu wa majengo na mjenzi.

Tunapenda kutoa shukrani zetu za dhati kwa wale wote waliofanya kazi na kushirikiana na Baba Witmar katika utume wake. Tunashukuru kwa namna ya pekee uongozi wa Majimbo ya Mtwara, Lindi na Pemba huko Msumbiji kwa kufanya nae utume kwa ushirikiano mkubwa. Pia tunashukuru viongozi wa Serikali walioshirikiana naye na hata kumshauri Pd. Witmar katika kazi zake za ujenzi. Pia serikali ya Mkoa wa Cabo Delgado (Msumbiji) kwa ushirikiano walioutoa ili kufanikish utume wake.

Tunawashukuru Masista wa Ndolo pale Imbuho Msumbiji. Walimtunza kwa upendo wa hali ya juu sana hasa alipoanza kudhoofika kimwili. Tunawashukuru kwa namna ya pekee Masista wa Tutzing hapa Ndanda kumpokea katika nyumba ya wazee na kumtuza kwa huruma na upendo mkubwa. Tunashukuru wafanyakazi wote katika nyumba hii ya wazee walivyo jitoa kumtunza. Tunawashukuru Madaktari na wauguzi wote waliomsaidia Baba Witmar hadi dakika ya mwisho. Mungu awabariki wote.

Baba Witmar amefariki akiwa na umri wa miaka 91 ya kuzaliwa. Miaka 71 ya utawa, miaka 66 ya upadre na miaka 62 ya umisionari hapa Tanzania. Hakufukia talanta zake. Hakika Bwana wa Mavuno atamwambia “vema mtumishi mwema na mwaminifu ulikuwa mwaminifu kwa machache nitakuweka juu ya mengi. Ingia katika furaha ya Bwana wako” Mt. 25:21

 

Apumzike kwa Amani!