“Nimevipiga vita vilivyo vizuri, mwendo nimeumaliza, imani nimeilinda.“  2 Tim 4:7

Maneno hayo yametimia tarehe 24 April 2021, hapo Mwenyezi Mungu alipomemuita kwake mtumishi wake Baba Ulrich Stöckl OSB atika makao ya milele, katika Hospital yetu hapa Ndanda. Pd. Ulrich alizaliwa huko Pessenburgheim Ujerumani tarehe 24 Mei 1924.  Katika familia yao walikuwa jumla ya watoto kumi – saba wa kiume na watatu wa kike. Alipobatizwa alipewa jina la Vitus.  Mmoja kati ya kaka zake alikuwa pia mtawa wa St. Ottilien. Huyu alijulikana kwa jina la Bruda Vulmar.

Pd. Ulrich baada ya kuwa mtawa na kutumwa Ndanda,  alifanya utume katika sehemu mbalimbaliwa kwa takribani miaka 50. Mwaka 2009, aliarudi hapa Ndanda na kusema “nimerudi nyumbani Ndanda kujianda kwa safari ya kwenda Mbinguni”  Kama sehemu ya maandalizi hayo, Pd. Ulrich aliandika historia fupi ya maisha yake ili isomwe siku ya mazishi yake:

“Nilizaliwa tarehe 24 Mei 1924 na kukua huko Pessenburgheim Ujerumani. Nilikulia katika familia ya ndugu 10. Wakiwemo kaka sita na akina dada watatu.  Tarehe 1, Mei 1930, niliingia shule ya msingi huko Holzeim. Miaka mitano baadaye, 1935 nilifanya na kufaulu mtihani wa kuingia seminari huko St. Ottilien. Hatimaye Serikali ya Kijerumani wakati huo ilifunga seminari zote ikiwepo ya St. Ottilien. Hivyo nikaingia chuo huko Dillingen. Chuo hiki vile vile kilifungwa tarehe 29 Aprili 1941, baada ya kuanza kwa vita ya Pili ya dunia mwaka 1939. Hivyo ilibidi niishi kwa dada wa Paroko wa Holzeheim, jina lake  Dora Häfele. Hali hii ilikaribia kuzima ndoto yangu ya kuwa mtawa na mmisionari. 

Mnamo Januari 1943 nilazimishwa na serikali Kijerumani kujiunga na jeshi kikosi maalumu cha kupigana vita milimani. Hivyo nikateuliwa kwenda Ufaransa kwa mafunzo hayo.  Hatimaye Juni 1943 nikapelekwa vitani Urusi. Nilikuwa vitani 1943 hadi mwisho wa vita mwaka 1945. Na katika kipindi hiki nilinusirika kifo na kujeruhiwa mara tatu. Nilipigwa rasasi kadhaa na moja ilibakia mwilini mwangu na kutolewa katika hospital na Ndanda na Dr. Mwambe mwaka 1999. Hivyo kuanzia mwaka Mei  1945 hadi Julai 1949 nilikuwa mfungwa wa kivita huko  Gorki, Urusi.

Baada ya kuachiwa huru Julai 1949, miezi mitatu baadaye yaani Octoba 1949, niliingia tena St. Ottilien na kuendelea na maisha ya wito kwa kusoma Falsafa na Tauhidi. Baada ya kumaliza masomo tarehe 7 Agosti 1955, nilipewa daraja la upadre. Na nilisoma misa yangu ya shukrani huko Pressenbyrgeheim, tarehe 14 Agosti 1956.

Novemba 1956 nilitumwa London, Uingereza kujifunza lugha ya Kingereza kwa muda wa miezi sita . Hatimaye nikarejea St. Ottilien na mwaka 1957 nilitumwa misioni hapa Ndanda. Hapa Ndoto yangu ya kuwa Mtawa, Padre na Mmisionari ilitimia. Namshukuru Mungu

Nikiwa mmisionari hapa Ndanda nilifanya utume sehemu zifuatazo.  

  • Mwaka 1957 – 1959 nilikuwa paroko msaidizi huko Mnero
  • Mwaka 1960 – 1962 nilikuwa Paroko huko Nanyamba
  • Mwaka 1962 – 1985 nilikuwa Paroko Ndanda
  • Mwaka 1985 – 1999 nilikuwa Paroko huko Chinongwe
  • Mwaka 1999 – 2005 nilikuwa Paroko huko Chigugu
  • Mwaka 2005 – 2015 nilikuwa baba wa Kiroho kwa Masista wa B.M.M.W Ndanda

Katika hayo yote namshukuru Mungu kwa ulinzi wake. Ameniepusha na hatari nyingi sana katika maisha yangu na amenifanikisha katika mengi. Mama Bakira Maria alinibeba daima katika mikono yake. Sikupata shida au mahangaiko ya kudumu katika maisha yangu. Ninaweza tu kusema: Asante Mungu.”

Baba Ulrich katika maisha yake ya kimisionari hapa Tanzania, alifanya utume wake kwa moyo wake wote, kwa nguvu zake zote na kwa akili yake yote. Mara moja vijana walimuuliza Baba Ulrich umeshawahi kufika Abasia ya Peramiho? Akajibu sina nafasi maana nilikuja Afrika si kutalii au kufanya picnic. Nillikuja kufanya utume. Hivyo siwezi kuacha utume na kwenda huko. Mwisho akasema nitaiona Peramiho nikiwa mbinguni.

Baba Ulrich alipokuwa Parokiani alisisititiza sana utume wa Legio Maria. Alisema Maria ni kimbilio na mlinzi wa kila shida. Hivyo kila Parokia aliyokuwepo utume wa Legio Maria ulikuwa juu. Pia alisisitiza sana  miito mitakatifu na kulea miito ya Upadre na utawa wa kike na kiume. Chini yake kama Paroko maparokia mbalimbali, vijana kumi na saba waliweza kuwa mapadre na baadhi yao wako hapa leo hii. Wao ni mashahidi. Katika Parokia ya Ndanda pekee kuna vijana 9 walikuwa mapadre  chini ya uongozi wake akiwemo hayati Askofu Gabriel Mmole. Kwa hakika mapadre na watawa hawa waliolelewa na Baba Ulrich wana deni kubwa la kumwombea na  kuiga mfano wa maisha yake. Alisisitiza sana na kushauri maisha ya Ndoa. Alikemea Ndoa za kifahari na kukemea wazazi waliodai mahari ya bei kubwa. Alisema mahari ya bei kubwa ni ULANGUZI  wa Ndoa. Pia Baba Ulrich alianzisha vituo vya afya na shule za Chekechea katika maparokia alimokaa.

Baada ya miaka ya 50 utume wake wa kimisionari, Baba Ulrich alirudi rasmi Abasia na kushirika maisha mazima ya kitawa. Alikuwa mfano wa kuigwa  kila mahali. Akiwa na miaka zaidi ya 95 bado alishirika mazoezi ya kuimba ya Jumuia japo hakuwa na sauti tena. Lengo lilikuwa kuonesha mfano kwa vijana. Alikuwa muungamishi na mshauri wa kiroho kwa watawa na hata mapadre wa majimbo. Alipokuwa maparokiani alijenga makanisa mengi ambayo siku hizi ni Parokia katika Majimbo ya Lindi na Mtwara. Pia alikuwa fundi wa kukarabati typewriter na makanisa yaliyo bomoka likiwepo kanisa la St. Fransis huko Lindi Mjini na huko Lushoto jimboni la Tanga.

Leo kwa hakika tunaweza kusema Ndanda tumempoteza mtawa, padre na mmisionari wa kuigwa katika maisha yetu. Ametufunza mengi na tumejifunza mengi kutoka kwake. Lakini kwa macho ya kiimani bado tupo naye kwani ni mwombezi wetu. Tuyaishi, tuyaenzi na tuyadumishe yale aliyotufundisha na tuliyoona kwake. Hiyo ndiyo heshma yetu kwa Baba Ulrich.

Kutokana na hayo yote hatuna shaka kwamba Baba Ulrich ataambiwa “vema mtumishi mwema na mwaminifu, ingia sasa katika makao uliyotayarishiwa”  Pd. Ulrich amefariki akiwa na umri wa miaka 97, miaka 71 ya utawa, miaka 66 ya upadre na miaka 64 misioni hapa Ndanda/Tanzania.

Raha ya milele umpe  Ee Bwana. Na mwanga wa milele umwangazie. Apumzike kwa amani. Amina