Kufuatia uchaguzi wa Pd. Christian Temu OSB hapo Machi 25 2021 kama abate wa Sita wa monastery ya Ndanda, sherehe ya kumsimika rasmi imefanyika katika viwanja vya abasia tarehe 8 Juali 2021.

Sherehe hiyo ya kufana ilikuwa na sehemu mbili: adhimisho la Misa ambalo wakati linaendelea abate mpya alipokea baraka rasmi ya kiabate; na sehemu ya mashangilio ambayo hotuba, nasaha na maburudisho mbalimbali yalitolewa.

Katika sherehe hii Wanaabasia walibarikiwa kuungwa mkono na maaskofu kadhaa. Kwanza kabisa ni askofu Titus Mdoe (Mtwara), askofu Bruno Ngonyani (Lindi), askofu Philbert Mhansi (Tunduru-Masasi) na askofu John Ndimbo wa jimbo la Mbinga.

Maabate na ndugu Wabenediktini kutoka sehemu mbalimbali, pia, walihudhuria tukio hili adimu: Abate Mkuu wa St. Ottilien Wolfgang Öxler, abate Aloysius Altman wa Koenigsmuenster na abate mstaafu Anastasius Reiser – wote wa Ujerumani. Maabate wa Afrika waliohudhuria na abate Pambo Martin (Mvimwa), abate Octavian Masingo (Hanga), abate Romain Botta (Agbang, Togo), abate John Baptist w  (Tigoni, Kenya), abate mstaafu Thadei Mhagama (Hanga) na Pd. Melchior Kayombo – priori wa Peramiho.

Kwa kuchaguliwa, kuthibitishwa na sasa kupokea baraka ya kiabate – mchakato wa kurudisha uongozi katika abasia ya Ndanda baada ya kifo cha abate aliyetangulia umekamilika.

Akitoa nasaha zake mwishoni mwa sherehe hiyo, Abate Christian aliwashukuru viongozi wa kiserikali, wa kikanisa, wa shirika lake na pia wadau wote wa kazi za kimisionari kwa mshikamano wanauonesha na hivyo kuiwezesha Ndanda kutekeleza majukumu yake ya kimisionari kwa ufanisi. Chini ya uongozi wake, abate mpya amesema, Ndanda – kwa kushirikiana na wadau wengine wa maendeleo na wa mambo ya kimisionari – itaendelea kuwa mdau wa kuaminika katika kuchochea maendeleo ya kimwili na hasa ya kiroho kwa watu wetu; iwe hapa Tanzania au kule Msumbiji ambako misioni mpya ilifunguliwa hapa karibuni.

Yamekuwa maadhimisho mazuri na yaliyofana. Na hapa abasia  Ndanda inawashukuru wale wote ambao kwa sala, muda, zawadi na matashi yao mema wamefanya tukio hili lifanikiwe.

Sherehe zimeisha na sasa kazi inaanza!