TAREHE  25. 3. 2021, Raisi wa Shirika la Wabenediktini Wamisionari duniani alitoa taarifa ifuatayo:

“Baada ya kifo cha aliyekuwa abate wa Ndanda Pd. Placidus Mtunguja OSB hapo Machi 2, 2021, watawa wa Ndanda wamemchagua

Pd. Christian Temu OSB

ambaye ni mtawa na mmisionari wa abasia kuwa abate wa sita wa Monasteri hiyo. Kwa sasa Pd. Christian anafanya utume wake nchini Ujerumani kama Mtendaji Mkuu wa Misioni wa Shirika.”

Uchaguzi huu umefanyika kuziba pengo lililoachwa na mpendwa abate wetu Placidus Mtunguja OSB aliyefariki baada ya kuugua muda mfupi mwanzoni mwa mwezi Machi 2021. Baada ya maombelezo ya tarkiban wiki tatu, jumuiya ya abasia imekaa na kutafuta njia jinsi gani maisha yaendelee. Baada ya matayarisho ya namna mbalimbali, jumuiya imekata shauri kumchagua Pd.  Christian Temu OSB kuwa abate wa sita wa abasia ya Ndanda. Hadi wakati wa kuchaguliwa kwake, Pd. Christian amekuwa anafanya kazi katika ofisi kuu ya Shirika huko Ujerumani kama Mtendaji wa Misioni.  Kwa uchaguzi huu, abasia inafungua ukurasa mpya katika historia ya viongozi wake. Baba Abate Placidus ataendelea kukumbukwa kwa upando na shukrani kwa mchango wake mkubwa kwa jumuiya yetu.

Kila kizazi kinasimama juu ya mabega ya kizazi kiilchotangulia. Abate mpya naye anasimama juu ya mabega ya watangulizi wake ambao walifanya kazi nzuri ya kuijenga jumuiya imara ya kimonaki na kimisionari. Hadi siku ya uchaguzi jumuiya ya abasia imekuwa na jumla ya watawa 92. Wengi wao wanaishi, kusali na kufanya kazi ndani au karibu na abasia. Wengine kati yao wanakaa katika nyumba ndogo za Sakharani na Dar es Salaam. Kuna idadi nzuri ya wanafunzi wanaosoma nchini Tanzania, Kenya, Msumbiji na Zambia. Wengine wanasoma mbali zaidi: Amerika ya Kusini (Brazili) na Korea Kusini. Wote hawa – walioko mbali na karibu; wanaofanya kazi na walioko masomoni watakuwa ni nguzo na mwamba wa kumtegemeza Abate mpya katika majukumu yake.

Jumuiya za kibenediktini zina tabia ya kutokubadilika-badilika. Wabenediktini wanadumu katika yale wanayofanya – iwe namna ya kusali, ya kufanya kazi na hata aina ya kazi au utume wanaofanya. Katika uongoozi mpaya huu pia, ingawa bado ni mapema mno kusema, tunaweza kuhisi kwamba mrithi wa Abate Placidus ataendeleza na kuimarisha ile mipango ambayo jumuiya imeshwajiwekea tayari. Bila juhudi zitaendelea katika kuimarisha roho ya kimonaki na ya kimisionari katika abasia. Tunaweza kutegemea pia kwamba, abate mpya ataendeleza na kuimarisha utume wa abasia katika sekta za afya, elimu na uchungaji kwa ujumla. Pia utume mwingine muhimu kabisa ni misioni ya Msumbiji.  Misioni hii ya Msumbiji ni inawezwa kutajwa „mradi mkakati.“ Ndugu wa abasia zaidi ya watano wanahusika moja kwa moja na misioni hii. Tutegemee kwamba, mara baada ya hali ya usalama itakavyoruhusu, abate mpya atasimamia kwa nguvu utekelezaji wa kazi hii ya kimisionari.

Abasia ya Ndanda imeendelea kupiga hatua katika maisha yake ya ndani na utume wake wa nje, siyo tu kwa sababu ya juhudi za watawa wenyewe, bali hasa kutokana na uwepo wa majirani wema na marafiki wengi wa nje na ndani ambao kwa sala na sadaka zao wamekuwa wanatuimarisha. Hatuna shaka basi, kwamba hata katika kipindi hiki kipya cha uongozi, uwepo wa majirani na marafiki zetu – wa mbali na wa karibu – utaendelea kutuimarisha katika wito wetu kama watawa na wamisionari.